Jumatano 18 Novemba 2026 - 20:00
Wanazuoni na Vijana wa Bahrain Wanakamatwa na Kuteswa kwa Sababu ni Mashia/ Hukumu za Kifungo cha Maisha Zatolewa Dhidi ya Wanazuoni wa Bahrain

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khujasteh amesema kuwa idadi kubwa ya wanazuoni, viongozi wa dini na vijana wa Bahrain wamekamatwa na kuteswa kutokana na kupinga sera za utawala na kulalamikia hatua zake.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad Khujasteh, mwalimu wa Hawza ya Kielimu ya Bahrain, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumzia matukio ya hivi karibuni nchini humo na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanazuoni wa Kishia, alisema: "Kinachoendelea leo nchini Bahrain si suala la kuwafungulia mashtaka watu wachache wa kidini pekee, bali kwa hakika ni kuyafungulia mashtaka madhehebu ya Kishia pamoja na vipengele na nyanja zote zinazounda utambulisho wa kidini wa Mashia wa nchi hii. Hii ni kwa sababu utawala wa Aal Khalifa umeanza kuchukua hatua za kuibana jamii ya Kishia na kukandamiza utambulisho wake wa kidini na kimadhehebu."

Aliongeza kuwa; baada ya vita vya uchokozi vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, utawala wa Aal Khalifa umeshindwa tena kuvumilia nafasi na heshima ya madhehebu ya Kishia. Kwa mtazamo wetu, kwa msaada na uungwaji mkono wa Wazayuni, utawala huo umeanzisha mpango wa kuongeza mashinikizo na kuishambulia jamii ya Kishia nchini Bahrain.

Kukamatwa na kuteswa wanazuoni na vijana wa Bahrain

Mwalimu huyo wa Hawza ya Kielimu ya Bahrain, akieleza kuwa mpango huo ulianza kwa kukamatwa Mashia na kuwekewa vikwazo mbalimbali dhidi yao, alisisitiza: "Katika hatua za mwanzo, watu waliokosoa mashambulizi ya Marekani yaliyofanywa kutoka katika ardhi ya Bahrain walikamatwa mitaani. Aidha, kila aina ya kutoa maoni, kupinga sera za utawala au kueleza mitazamo tofauti ilikabiliwa na hatua za kiusalama, kukamatwa na kuteswa."

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khujasteh aliendelea kusema: "Idadi kubwa ya wanazuoni, viongozi wa dini na vijana wa Bahrain wamekamatwa na kuteswa kutokana na kupinga sera za utawala na kulalamikia hatua zake. Miongoni mwa mifano ya kusikitisha ya vitendo hivyo ni tukio la Sayyid Muhammad Mousawi, ambaye kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, aliuawa kjshahidi wakati wa kuteswa."

Akizungumzia kuongezeka kwa mashinikizo dhidi ya viongozi wa kidini na wanazuoni wa Hawza nchini Bahrain, alisema kuwa utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukiwafuatilia wanazuoni, Maimamu wa Swala za Ijumaa na jamaa pamoja na walimu wa Hawza ya Kielimu, kwa visingizio mbalimbali kama vile kueneza nadharia ya Wilayat al-Faqih, na tuhuma za kuwa na uhusiano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kudhibiti taasisi za Kishia na kuwekea vikwazo mijadala ya kidini

Mwalimu huyo wa Hawza ya Kielimu ya Bahrain, akizungumzia hatua za utawala wa Aal Khalifa za kutaka kudhibiti taasisi za kidini za Kishia, alisema: "Utawala wa Bahrain umedhibiti taasisi za Kishia, zikiwemo taasisi zinazohusiana na masuala ya wakfu. Sambamba na hatua hiyo, umeweka sheria ya kusimamia na kuwekea vikwazo mijadala na maelezo ya kidini."

Aliongeza kuwa hatua hizo zinachukuliwa katika mazingira ambayo taasisi za kidini na viongozi wa dini wa Kishia ni sehemu muhimu ya muundo wa kijamii na kiutamaduni wa jamii ya Bahrain. Hivyo, kuwekea vikwazo shughuli zao kwa vitendo kunamaanisha kubana uwezo wa kidini na kijamii wa sehemu kubwa ya wananchi wa nchi hiyo.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khujasteh, akikosoa mwenendo wa kushughulikia kesi za wanazuoni wa Kishia, alisema: "Mashauri yanayoendeshwa hivi sasa hayazingatii vigezo vya kisheria na haki ya kimahakama, wala hayalingani na hata misingi ya msingi kabisa ya kibinadamu na kisheria. Kuna hata taarifa zinazoeleza kwamba baadhi ya wanazuoni wamelazimishwa kusaini mambo ambayo kimsingi hawakuwa wameyaona wala kuyasoma."

Kesi za siri na kuwanyima watuhumiwa haki ya kujitetea

Akifafanua kile alichokiita mwenendo usio wazi wa kesi zinazowahusu wanazuoni wa Bahrain, alisema: "Kesi hizi zinaendeshwa kwa siri na bila kuutaarifu umma. Katika baadhi ya mazingira, hata watuhumiwa wenyewe hawahudhurii vikao vya mahakama."

Mwalimu huyo wa Hawza ya Kielimu ya Bahrain aliendelea kusema: "Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, miongoni mwa vielelezo muhimu zaidi vilivyowasilishwa dhidi ya watu hawa ni maelezo ya afisa mmoja wa usalama ambaye hakufichua utambulisho wake, na ambaye hata hakuwa na uelewa wa dhana za msingi kabisa zinazohusiana na tuhuma zilizotolewa."

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khujasteh aliongeza: "Maafisa wa utetezi walipomuuliza afisa huyo kuhusu maana ya Wilayat al-Faqih, jibu pekee alilolitoa lilikuwa kutamka neno 'Iran'. Kwa mujibu wa maelezo yake, jibu hilo ndilo lililotumiwa kama hoja katika mwenendo wa kesi dhidi ya wanazuoni wa Kishia."

Akizungumzia namna majaji wanavyoshughulika na watuhumiwa, alisema: "Mawasiliano kati ya majaji na baadhi ya wanazuoni yalifanyika kupitia mazungumzo ya video. Katika baadhi ya matukio, wanazuoni hao walipotaka kujitetea na kufafanua mitazamo yao, walinyamazishwa." Kwa mtazamo wetu, mwenendo wa namna hii unaonesha kuwa watuhumiwa hawakupewa fursa ya kujitetea ipasavyo, na kwamba hukumu za kisiasa zilikuwa tayari zimeamuliwa dhidi yao kabla ya kesi kuendeshwa.

Kesi dhidi ya wanazuoni wa Kishia ni kesi dhidi ya utambulisho wa kidini wa jamii ya Bahrain

Mwalimu huyo wa Hawza ya Bahrain, akisisitiza kuwa wigo wa hatua zinazochukuliwa hivi karibuni ni mpana zaidi kuliko kesi chache za mahakamani, alisema: "Kinachoendelea leo nchini Bahrain si kuwafungulia mashtaka wanazuoni wachache tu, bali ni kuifungulia mashtaka jamii nzima ya Kishia ya nchi hii. Jamii ambayo inakabiliwa na mfululizo wa vikwazo vya kidini, ukamataji na mashinikizo yaliyopangwa kwa utaratibu maalumu."

Alisisitiza: "Wakati wanazuoni, Maimamu wa Swala za Ijumaa na jamaa, walimu wa Hawza za kielimu na vijana wanapofuatiliwa na vyombo vya dola kwa sababu ya kueleza mitazamo yao ya kidini au kupinga sera za utawala, kwa hakika sehemu kubwa ya utambulisho wa kidini na kijamii wa jamii hiyo ndiyo inayolengwa."

Hukumu za kifungo cha maisha dhidi ya wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Khujasteh, akilaani hukumu zilizotolewa dhidi ya wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, hususan hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Ayatullah Sheikh Isa Qasim, alisema: "Sisi tunalaani hukumu za kifungo cha maisha zilizotolewa dhidi ya kundi la wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain, hususan hukumu ya kifungo cha maisha dhidi ya Ayatullah Isa Qasim." Alisema kuwa hukumu hizo zimetolewa chini ya ushawishi wa mashinikizo na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni pamoja na Saudi Arabia. Kwa mtazamo wetu, hatua hizo zinalenga kudhoofisha nafasi na hadhi ya wanazuoni wa Kishia, na kuzuia uwepo wao pamoja na mchango wao katika jamii ya Bahrain.

Mwalimu huyo wa Hawza ya Kielimu ya Bahrain, katika hitimisho la mahojiano yake, alisisitiza: "Wananchi wa Bahrain na Mashia wa nchi hii hawakubali hukumu za namna hii, na wanazilaani. Jamii ya Kishia ya Bahrain inataka mashinikizo na vikwazo vya kidini vikomeshwe, pamoja na kuheshimiwa haki za wanazuoni wa dini na wananchi wa nchi hii."

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha